N

NEMC Yapewa Agizo Kuhusu kiwanda cha mifuko ya viroba.

Baraza la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (Nemc), limeagizwa kuvipitia upya vibali vya kazi vya kiwanda cha kutengeneza mifuko ya viroba cha Anbangs ili kujiridhisha kama ni halali.
Agizo hilo lilitolewa jana na Naibu Waziri wa Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Luhaga Mpina wakati alipofanya ziara kwa mara ya pili katika kiwanda hicho sanjari na kuangalia uharibifu wa mazingira katika Bonde la Mto Msimbazi.
Mpina aliwaambia wanahabari jana kuwa mwaka jana alifanya ziara katika kiwanda hicho na aliagiza mambo manne ambayo hayakutekelezwa na wahusika wa kiwanda hicho kinachomilikiwa na Wachina.
Kati ya mambo hayo ni kufanya tathimini ya athari za mazingira, kupeleka vibali vya kufanya shughuli hizo, kulipa faini ya Sh25milioni kwa kosa la kutiririsha majitaka mtoni.“Imeshakuwa mazoea nikija hapa mnajifajifanya hamjui lugha na mnasingizia menejimenti haipo. Sasa leo Nemc hakikisheni mnavipata vibali vyao kama vipo na kama hakuna, kiwanda hiki ndani ya wiki moja kifungwe.“Kuhusu faini Nemc kaeni na menejimenti mjiridhishe kama kweli wamelipa, maana kila tukija hapa hawapo. Kama hawajalipa wapelekwe mahakamani kwa kukaidi amri halali iliyotolewa, mfanye kazi hii ndani ya siku saba,” amesema Mpina ambaye pia ni Mbunge wa Kisesa.
Mratibu wa Nemc, Japhar Chimgege aliliambia gazeti hili kuwa watafanya kama walivyoagizwa na waziri huyo na kwamba wamiliki wa kiwanda hicho wamekuwa wakikaidi amri halali iliyotolewa na Serikali.
Akizungumza kwa niaba ya uongozi, fundi wa mitambo wa kiwanda hicho, Twaha Salehe alisema baadhi ya maelekezo yaliyotolewa yamefanyiwa kazi ikiwamo ujenzi wa uzio na chemba ya kuweka majitaka.

Leave a Reply