97870400 Caffb242 F3a1 4b26 91fc D035de61bd66

Zarika Aelekea Marekani Kujiandaa Kwa Pigano Dhidi Ya Mzambia.

Bingwa wa dunia uzani wa super-bantam chama cha WBC, Fatuma Zarika wa Kenya, ameondoka siku ya Jumanne kuelekea Las Vegas, Marekani, kwa mazoezi ya kujiandaa kutetea ubingwa wake dhidi ya Catherine Phiri wa Zambia mwezi Disemba tarehe mbili mwaka huu jijini Nairobi.

Zarika, mwenye umri wa miaka 31, alitwaa ubingwa huo mwaka jana mwezi wa kumi nchini Marekani alipomshinda kwa pointi Alicia Ashley wa Jamaica.

Hii itakua mara ya kwanza kwa Zarika kutetea ubingwa wake. Ameshinda mapigano 29, 17 kwa KO, akapoteza mara 12 na kwenda sare mara mbili.

Catherine, mwenye umri wa miaka 30, ni bingwa wa zamani wa dunia mkanda wa WBC uzani wa bantam.

Alitwaa ubingwa wa dunia mwezi Januari mwaka jana kwa kumshinda Yazmin Rivas wa Mexico, na akapoteza taji hilo mwezi wa nne mwaka huu aliposhindwa kwa pointi na Mariana Juanez.

Catherine ameshinda mapigano 13, saba kwa KO na akashindwa mara mbili.

Akieleza ni kwa nini anasafiri Marekani kwa mazoezi, Zarika ambaye maneja wake sasa ni Ejay Matthews wa Marekani, anasema kule kuna vifaa vya kisasa na mabondia wa hadhi ya juu wa kufanya nao mazoezi.

“Nikiwa huko najifunza mengi sana kutoka kwa mabondia hao. Nyumbani sehemu nyingi tunakofanyia mazoezi hamna jukwaa, tunapigana sakafuni, na tena nikiwa ng’ambo hamna usumbufu kama hapa nyumbani,” asema Zarika.

Leave a Reply