S (26)

RAIS MAGUFULI AMEWAAPISHA DKT FARAJI KASIDI NA HAJAT MWANTUMU MAPEMA JANA

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo amemuapisha Dkt. Faraji Kasidi Mnyepe kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Hajat Mwantumu Bakari Mahiza kuwa Skauti Mkuu Tanzania.

Hafla ya kuapishwa kwa viongozi hao imefanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa Skauti Wabunge Tanzania Mhe. Job Yustino Ndugai, Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili na Mdhamini wa Chama cha Skauti Tanzania Alhaji Dkt. Ali Hassan Mwinyi, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia na Rais wa Chama cha Skauti Tanzania Prof. Joyce Ndalichako,Makatibu Wakuu na viongozi wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama.

Akizungumza baada ya kuwaapisha, Mhe. Rais Magufuli ambaye ni Mlezi wa Skauti Tanzania amekipongeza Chama cha Skauti Tanzania kwa kazi nzuri kinayoifanya ya kuwalea vijana kuwa wazalendo, kusaidia jamii hasa wakati wa matukio mabaya na majanga, kuwajengea tabia njema na kuwa na upendo.

Pamoja na kutoa pongezi kwa Skauti wote nchini, Mhe. Rais Magufuli amesema Serikali inatambua changamoto mbalimbali zinazowakabili na kwamba ipo tayari kushirikiana nao kuzitatua.

Amempongeza Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili Alhaji Ali Hassan Mwinyi kwa moyo wake wa upendo, unyenyekevu na jinsi anavyoendelea kushiriki katika shughuli za kijamii licha ya umri mkubwa alionao na amemhakikishia kuwa yeye na Watanzania wote wanampenda na wanamtakia kila la heri katika maisha yake.

Kwa upande wake mzee Mwinyi ameelezea kufurahishwa kwake na kazi nzuri inayofanywa na Rais Magufuli katika kuliletea Taifa maendeleo ambapo amemuomba Rais Magufuli kuendelea kuunga mkono juhudi zinazofanywa na chama hicho hapa nchini, na amewasihi viongozi wa Skauti Tanzania kufanya kazi zao kwa kuzingatia sheria, taratibu na kanuni za nchi.

Kwa upande wao Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dkt. Faraji Kasidi Mnyepe na Skauti Mkuu wa Tanzania Hajat Mwantumu Bakari Mahiza wamemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa kuwaapisha kushika nyadhifa hizo na wamemuahidi kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia viapo vyao, sheria, taratibu na kanuni za nchi.

Leave a Reply